Laiti kama Bunge juzi hapa lingepitisha mapendekezo ya Serikali juu
ya vipengele vya sheria ya magazeti ya 1976, basi, nayo ingelikuwa ni
habari nyingine ya huzuni kubwa kwa Watanzania. Ni habari ya aibu.
Kwamba miaka 50 baada ya Uhuru, pamoja na kuminyika sana kwa
wanahabari, bado kuna watendaji Serikalini wanaofikiria kuwaminya zaidi
wanahabari.
Ndio, bado kuna wanaofikiria Wanahabari hawa wenye kufanya kazi
kwenye mazingira magumu sana wapewe adhabu kali zaidi wanapofanya makosa
wakiwa kazini.
Na wakati mwingine inaonekana, kuwa mahusiano ya Serikali na
Wanahabari ni kama ya mzazi na mtoto. Kwamba Serikali ni mzazi, ambaye
kila anapoona mtoto amekosea, anachofikiria ni kutafuta bakora ya
kumchapa. Na mtoto anapoonekana kulifanya tena kosa, basi, mzazi
anafikirikia kuongeza idadi ya bakora. Ni mzazi anayetaka kutuhumu na
kuhukumu hapo hapo. Ni viboko tu. Hataki na haioni haja ya mtu mwingine
aingilie kati kuwasikiliza mzazi na mtoto kwenye kutofautiana kwao.
Na imeripotiwa kwenye Mwananchi, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), Jaji Frederick Werema juzi ameangukia pua baada ya Bunge kukataa
mapendekezo ya Serikali ya kubadili baadhi ya vipengele vya Sheria ya
Magazeti ya mwaka 1976, ya kuongeza adhabu kwa waandishi wa habari
watakaopatikana na hatia ya makosa ya uchochezi.
Mwananchi linaendelea kuandika, kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda,
aliungana na wabunge wengine kukataa mapendekezo hayo na kudai kuwa
wakati umefika kwa Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria ya vyombo
vya habari, badala ya kutoa ahadi zisizo na majibu kila wakati.
Kukataliwa kwa mapendekezo hayo ni pigo kwa Serikali na Jaji Werema
ambaye juzi wakati akijibu hoja za wabunge alijigamba kwamba yeye
anasimamia amani ya nchi kwa hiyo vifungu hivyo haviwezi kuondolewa,
kwani anafanya kazi kwa masilahi ya taifa na hategemei magazeti kwa
ajili ya kuwa mbunge. Ni kauli ambayo iliwachefua wabunge. Linaandika
gazeti Mwananchi, Ijumaa, Novemba 9, 2013.
Ndugu zangu,
Nahofia, kuwa wakati mwingine wanasiasa wetu wanatunga sheria kwa
kuziona 'hatari zilizo mbele yao' zinazotishia maslahi yao binafsi, ya
vikundi vyao na ya vyama vyao. Na wala si kwa hatari iliyo mbele yetu
kama taifa. Hivyo basi, kauli za kulinda maslahi ya taifa wakati
mwingine hutumiwa kama koti la kulivaa kuficha dhamira halisi za hao
wenye kuiona ' hatari iliyo mbele yetu'.
Tutafanya makosa kama taifa, kama tutafika mahali hata sheria zetu
tutakuwa tukizitunga kutokana na ' hofu' za kisiasa. Hofu za kisiasa ni
hisia za kuja na kupita, lakini, yenye kuhusu maslahi ya taifa ni mambo
tunayotakiwa kuyajengea msingi na yakabaki hata kama sisi hatutakuwepo
duniani.
Majuzi tu hapa alikuja Spika yule wa Bunge la Uswisi na akashangaa
kusikia kwenye nchi hii bado kuna magazeti yanafungiwa kwa sheria ya
mwaka 1976. Akatwambia kuwa kule kwao anakumbuka mara ya mwisho gazeti
kufungiwa ilikuwa ni baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Ndio, Wanahabari wa nchi hii si malaika, nao, kama wanataaluma
wengine, wanafanya makosa. Lakini tufike mahali, nasi tufikirie taratibu
nyingine za kusahihishana na kupeana adhabu bila kufikiria kwanza
adhabu za vifungo vya magerezani. Na kazi ya kusahihishana na kupeana
adhabu inaweza kabisa kuachwa kufanywa na wanahabari wenyewe kupitia
vyombo vyao husika vya kurekebishana na kuadhibiana. Ndivyo wanavyofanya
madaktari, mainjinia, walimu na wengineo. Ikishindikana huko ndiko
mahakama zitumike.
Maana, inasikitisha leo kuliona gazeti la Kitanzania likitoka huku
likionyesha siku ambazo zimebaki kabla ya gazeti dada kufunguliwa.
Maana, kwa maisha ya magazeti ya sasa, hakuna ajuaye amebaki na siku
ngapi kabla ya kufungiwa. Mungu tu ndiye ajuaye!
Na katika dunia hii tusiishi tukasahau kanuni za maisha. Kuwa kuna
kupanda na kushuka. Kuna leo na kesho. Ya leo unayajua na ya kesho
huyajui. Usiyemhitaji leo utamhitaji kesho. Ni kwa vile wewe ni
mwanadamu.
Na hapa nitamalizia na kisa cha Mbunge Eliakim Simpasa. Julai 3 mwaka
huu, wakati nikitembea kwa miguu Mtaa wa Shaaban Robert jijini Dar,
nilikutana na ndugu zangu wawili kwenye familia ya wanahabari; Boniface
Makene na John Mapinduzi. Wawili hawa nao walikuwa wakitembea kwa miguu
wakiongozana na Mbunge Mstaafu, Mzee Eliakim Simpasa. John na Boniface
kwa sasa wako Ofisi ya Makamu wa Rais.
Basi, tukaongea kidogo, na ilibaki kidogo tu nimkumbushe Mzee Simpasa
juu ya ugomvi wake na wanahabari, enzi hizo akiwa Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Haki na Maadili.
Maana, nakumbuka siku moja akiwa bungeni, Simpasa alimwomba Spika
amwamuru mwandishi wa habari, silikumbuki jina lake, aingie Bungeni na
ajieleze mbele ya Bunge juu ya habari potofu aliyoiandika juu ya ' Bunge
Tukufu'. Eliakim Simpasa alikuwa kama ' Dikteta' fulani hivi!
Naam, nilisita kumkumbusha Mzee Simpasa, maana, yawezekana mwandishi huyo alikuwa ni John Mapinduzi au Boniface Makene!
Na leo hii ndio hao anaotembea nao mitaani kwa miguu, kama ndugu!
0 comments:
Chapisha Maoni